Home Habari Kuu Hofu ya kuzuka kwa vita vikali kati ya Israel na Hezbollah yatanda

Hofu ya kuzuka kwa vita vikali kati ya Israel na Hezbollah yatanda

0
kra

Shambulizi la roketi katika uwanja wa kandanda katika mji unaokaliwa na Israel wa Golan Heights linalodaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Hezbollah, limezua hofu ya vita vikali kati ya Israel na Hezbollah.

Tangu vita kati ya Israel na Hamas vilipoanza Oktoba mwaka jana, Israel na Hezbollah zimekuwa zikichokozana kwa mashambulizi ya kiwango cha chini.

kra

Mashambulizi hayo madogo yamesababisha vifo vya watu kadhaa na kusababisha wengine wengi kuhama makazi yao katika pande zote mbili, Lebanon na Israel.

Watoto wapatao 12 wanaripotiwa kufariki kwenye shambulizi hilo la Jumamosi katika eneo la Majdal Shams kwenye mji wa Golan Heights, unaokaliwa na Israel.

Israel inalaumu Hezbollah kwa shambulizi hilo ikiahidi kulipiza kisasi, huku kundi la Hezbollah likikana kuhusika kwenye shambulizi hilo.

Katika taarifa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema kwamba Israel haitapuuza shambulizi hilo na kwamba kundi la Hezbollah litalipa kwa gharama ya juu.

Daniel Hagari, msemaji wa jeshi la Israel alisema kwamba ujasusi unaashiria kwamba roketi ya Jumamosi ilirushwa na wanachama wa kundi la Hezbollah kutoka Lebanon na hatua ya kundi hilo kukana ni uongo tu.

Madai ya Hagari yaliungwa mkono na waziri wa masuala ya kigeni wa Marekani Antony Blinken ambaye aliongeza kusema kwamba Marekani itaunga mkono Israel katika hatua itakazochukua kulinda wananchi wake dhidi ya mashambulizi kama hayo.

Tayari miili ya watoto waliofariki kwenye shambulizi hilo imezikwa.