Home Habari Kuu Hitaji la viza laondolewa kwa raia wa Indonesia wanaozuru Kenya

Hitaji la viza laondolewa kwa raia wa Indonesia wanaozuru Kenya

0

Rais William Ruto ametangaza kuondolewa kwa hitaji la viza kwa raia wa Indonesia wanaoingia Kenya mradi wana paspoti za nchi hiyo. Hii ni baada ya Rais Ruto kufanya mazungumzo na Rais wa Indonesia Joko Widodo anayezuru Kenya.

Haya yanajiri wakati ambapo Kenya na Indonesia zimetia saini mikataba minne ya maelewano na barua ya kuonyesha nia ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji kati ya nchi hizi mbili.

Akizungumza leo katika Ikulu ya Nairobi wakati wa kutia saini mikataba hiyo, Ruto alisema nchi hizo mbili zinaimarisha ushirikiano ili kunufaika na fursa zilizopo zinazolenga kusawazisha biashara kati yazo.

Rais Ruto na Rais Widodo walijadiliana pia kuhusu ushirikiano katika elimu ya juu, elimu ya msingi na utayarishaji chanjo.

Kutokana na hilo, bodi ya dawa na sumu nchini Kenya iliingia kwenye mkataba na mamlaka ya chakula na dawa ya Indonesia utakaofanikisha kuimarishwa na kutekelezwa kwa sera za kudhibiti bidhaa za dawa.

“Mkataba unaonzisha mpango kati ya Biovax ya Kenya na BioFarma ya Indonesia wa ushirikiano wa kubadilishana teknolojia, kutayarisha bidhaa, kusajili bidhaa, kusambaza na kuuza chanjo zitakazoundwa na BioFarma nchini Kenya umetekelezwa.” Alisema Rais Ruto.

Rais Ruto alimpa Rais Joko Widodo heshima inavyostahili kwa mizinga 21.

Katika ziara yake ya kwanza barani Afrika, Widodo atazuru Tanzania, Mozambique na Afrika Kusini.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here