Naibu Gavana wa kaunti ya Siaya William Oduol atajua iwapo atandelea kuhudumu katika wadhifa huo au la Jumatatu ijayo.
Bunge la Seneti litaandaa kikao maalum siku hiyo kujadili ripoti ya Kamati Maalum iliyoteuliwa kuchunguza tuhuma zilizowasilishwa na bunge la kaunti ya Siaya dhidi yake.
Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Seneta William Kisang imekuwa ikiandaa vikao vya kusikiliza tuhuma hizo kwa lengo la kuzipima mizani kubaini ikiwa bunge la kaunti ya Siaya lilikuwa na sababu za kutosha kumtimua Oduol.
Spika wa bunge la Seneti Amason Kingi kupitia gazeti rasmi la serikali amesema kikao cha kuijadili ripoti ya kamati hiyo kitaanza saa 8.30 alasiri Jumatatu ijayo.
Ikiwa bunge la Seneti litakubaliana na hatua ya bunge la kaunti ya Siaya, basi Oduol atakuwa Naibu Gavana wa kwanza kutimuliwa kutoka wadhifa huo tangu kuasisiwa kwa ugatuzi mnamo mwaka wa 2010.
Ikiwa Maseneta watapuuzilia mbali madai hayo, basi Oduol atakuwa na kila sababu ya kutabasamu akifahamu kuwa ataendelea kuhudumu katika wadhifa huo.
Oduol amekana tuhuma zote alizolimbikiziwa na bunge la kaunti ya Siaya ikiwa ni pamoja na utumiaji mbaya wa wadhifa wake na ukiukaji wa katiba.
Jana Alhamisi, alikana kuhusika katika ununuzi wa kiti kilichodaiwa kununuliwa kwa shilingi milioni 1.12.
Kiti hicho kilizua msisimko miongoni mwa maseneta wakati wa kikao cha Kamati Maalum ya Seneti iliyochunguza tuhuma dhidi ya Oduol.
Wawakilishi Wadi wote 42 wa bunge la kaunti ya Siaya waliazimia kumtimua Oduol kufuatia mapendekezo ya jopo la wanachamana 14 lililobuniwa kumchunguza.
Katika kuchukua hatua hiyo, walimtuhumu, kwa miongoni mwa mambo mengine, kukiuka katiba na kupotosha umma kwa kutoa taarifa za uongo.
Uhusiano mzuri ulioshamiri kati ya Gavana wa kaunti ya Siaya James Orengo na mgombea mwenza wake wakati huo William Oduol ulizorota kuanzia mwishoni mwa mwaka uliopita huku Oduol akimnyoshea Orengo kidole cha lawama kwa kukimya wakati kukiwa na ubadhirifu wa fedha za umma.