Hatima ya Naibu Rais Rigathi Gachagua itabainika katika kipindi cha siku saba zijazo ambazo zimetengwa kisheria kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi ya utovu wa nidhamu dhidi ya kiongozi huyo.
Kulingana na taarifa ya Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula Jumanne jioni mswada huo lazima utashirikisha maoni ya umma.
Maoni ya wananchi yataanza kupokewa Ijumaa, Oktoba 4 katika kaunti 47 kote nchini na kuwasilishwa bungeni kabla ya Jumanne ijayo.
Bunge litarejelea vikao vyake Jumanne saa tatu asubuhi hadi usiku wa manane, kujadili na kupiga kura kubaini hatima ya Rigathi.
Bunge pia limetangaza kufutilia vikao vyake kesho jioni ili kuruhusu umma kutoa maoni ya kubanduliwa kwa Naibu Rais.
Rigathi pia atahitajika kufika bungeni kujitetea binafsi au kupitia kwa mwakilishi wake Oktoba 8, kati ya saa kumi na moja jioni na saa moja jioni kabla ya uamuzi kutolewa.
Akisoma maagizo hayo, Wetang’ula amesema kuwa bunge litapendekeza kwa huduma ya kitaifa ya polisi kutoa usalama zaidi kwa wabunge waliounga mkono hoja hiyo hususan kutoka kwa eneo anakotoka Rigathi.
Endapo bunge la Kitaifa litapitisha kung’atuliwa kwa Naibu Rais, bunge la Seneti litakuwa na uamuzi wa mwisho wa aidha kupitisha ripoti hiyo au kuitupilia mbali.