Sherehe ya harusi ilgeuka na kuwa msiba huko Ruiru kaunti ya Kiambu, baada ya wanawake watano na mtoto mmoja kufariki kufuatia kuporomoka kwa shimo la maji taka.
Wageni hao wa harusi walikuwa wakicheza densi juu ya shimo hilo lililokuwa limefunikwa kwa zege wakati iliporomoka na wakatumbukia ndani.
Sita hao waliofariki walikuwa sehemu ya watu ambao walikuwa wamekwenda kumchukua bibi harusi kutoka nyumbani kwao katika eneo la Fort Jesus, Kihunguro, Jumamosi asubuhi.
Kamanda wa polisi katika kaunti ya Kiambu Perminus Kioi alielezea kwamba ufuniko wa shimo hilo uliokuwa umeundwa kwa zege ulizidiwa na uzani wa watu hao ambao walitumbukia humo.
Shughuli za uokozi zilianzishwa mara moja ambapo watu 11 wakiwemo watoto wawili waliokolewa na kupelekwa kwenye hospitali mbali mbali za eneo hilo la Ruiru.
Timothy Mbugua aliyekuwa kwenye kundi la kumchukua bibi harusi alielezea kwamba waliotumbukia kwenye shimo hilo ni watu 20.
Baada ya shughuli ya uokozi kukamilika, maharusi Charles Mworia na Susan Wanjira waliunganishwa kwenye ndoa takatifu katika kanisa la Wonders Touch Ministries International na baadaye maankuli katika uwanja wa shule ya wavulana ya Ruiru.
Ujenzi duni umelaumiwa kwa ajali hiyo.