Home Michezo Harambee Stars kurejea kambini wiki hii

Harambee Stars kurejea kambini wiki hii

Stars itacheza dhidi ya 'Panthers' ya Gabon katika uwanja wa Renovation Jijini Franceville tarehe 16 mwezi huu, kisha ichuane na Seychelles siku nne baadaye jijini Port Louis.

Timu ya taifa ya soka Harambee Stars.

Timu ya taifa ya soka, Harambee Stars inatarajiwa kuripoti kambini juma hili ili kujitayarisha kwa michuano ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026 dhidi ya Gabon na Ushelisheli.

Timu hiyo inayofunzwa na kocha Engin Firat, itazikosa huduma za kiungo Collins Sichenje, mlinzi tajika Brian Mandela, na Daniel Anyembe kutokana na jeraha na pia sababu za kibinafsi.

Sichenje, ambaye huchezea klabu ya AIK nchini Uswidi, atakosa mechi mbili kutokana na jeraha, ilhali Brian Mandela wa Mamelodi Sundowns hatashiriki kutokana na sababu za kibinafsi.

Wachezaji wanaosakata soka humu nchini wanatarajiwa kuripoti kambini juma hili katika uwanja wa Kasarani kabla ya timu hiyo kuelekea Gabon Novemba 13.

Harambee Stars itakwaruzana na “Panthers” ya Gabon katika uwanja wa Renovation jijini Franceville tarehe 16 mwezi huu, kisha ichuane na Ushelisheli siku nne baadaye jijini Port Louis.

Timu zingine katika kundi F ni Ivory Coast, Gambia na Burundi.