Home Kimataifa Hamas: Makubaliano ya kusitisha vita kwa muda yanakaribia

Hamas: Makubaliano ya kusitisha vita kwa muda yanakaribia

0

Mapigano yaliendelea leo Jumanne katika Ukanda wa Gaza, zaidi ya wiki sita baada ya shambulizi lililotekelezwa na kundi la Hamas kuichochea Israel kufanya mashambulizi ya angani na ardhini.

Israel imeapa kuwaangamiza wanamgambo wa Palestina.

Katika Ukanda wa Gaza, watu zaidi ya 13,300, angalau 5,600 kati yao watoto, wameuawa katika mapigano hayo, maafisa katika eneo linaloendeshwa na Hamas wanasema.

Watu wapatao 1,200, wengi wao raia, waliuawa nchini Israel wakati wa shambulizi la Oktoba 7 na wengine wapatao 240 kutekwa nyara, kulingana na maafisa wa Israel.

Kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh alisema leo Jumanne kuwa makubaliano ya kusitisha vita kwa muda yanakaribia kufikiwa, na kuibua matumaini kwamba makumi ya watu waliotekwa nyara wataachiliwa huru.

“Tunakaribia kufikia makubaliano ya kusitisha vita,” alisema Haniyeh, kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na ofisi yake kwa AFP.

Chini ya makubaliano hayo, kati ya raia 50 na 100 wa Israel na mateka wa kigeni wanaweza wakaachiliwa huru, lakini sio wanajeshi.

Katika mabadilishano, Wapalestina wapatao 300 wataachiliwa huru kutoka magereza ya Israel, miongoni mwao wanawake na watoto.

Israel haikujibu hilo mara moja.

Jana Jumatatu, Rais wa Marekani Joe Biden alisema anaamini makubaliano hayo yanakaribia huku Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundi akiashiria kuwa Rais wake amesafiri kuelekea Qatar kukutana na kiongozi wa Hamas.