Home Biashara Halmashauri ya KRA yazindua mnada mtandaoni

Halmashauri ya KRA yazindua mnada mtandaoni

Aidha halmashauri ya  KRA ilisema itaendelea kutumia teknolojia kuhakikisha uzingatiaji sheria kuhusu ushuru.

0

Halmashauri ya ukusanyaji ushuru hapa nchini KRA, imezindua mnada wa mtandaoni, kama sehemu ya kulainisha taratibu za usimamizi kuhusu ushuru.

Kwa mujibu wa KRA, hatua hiyo inalenga kuimarisha utoaji huduma na pia kuboresha ukusanyaji ushuru.

Akitangaza uzinduzi huo siku ya Jumatatu, Kamishna Mkuu wa KRA Humphrey Wattanga,  alisema hatua hiyo ilifuatia ufanisi wa majaribio ya mnada mtandaoni ambapo ilikusanya shilingi milioni 37.5.

“Hatua hiyo itapiga jeki juhudi za serikali za kuondoa msongamano bandarini, na itahakikisha mizigo inashughulikiwa kwa wakati,” alisema Wattanga.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwezi kuhusu ulipaji ushuru Jijini Mombasa, Wattanga alidokeza kuwa  mnada huo wa mtandaoni, utawapa walipa ushuru fursa ya kufurahia mfumo ulio na uwazi wa kushugulikia zabuni.

Kamishna huyo mkuu alisema halmashauri ya KRA, Kwa sasa imejitolea kufanikisha mpango utakaowezesha walipa ushuru kuzingatia sheria za KRA, huku akiwataka walipa ushuru kukumbatia mpango huo kabla muda wake kukamilika tarehe 30 mwezi Juni mwaka 2024.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa fedha na mipango ya uchumi Prof Njuguna Ndung’u, alisema mpango wa kutoa msamaha kwa walipa ushuru, ni miongoni mwa sera za serikali zinazolenga kuwakinga wakenya dhidi ya changamoto  zinazoshuhudiwa hapa nchini na kimataifa.

“Mpango wa kuwasamehe walipa ushuru, unalenga kuongeza mapato kwa kuwa walipa ushuru watalipa kwa hiari fedha ambazo hazingekusanywa na serikali,” alisema Waziri Njuguna.

Aidha halmashauri ya  KRA ilisema itaendelea kutumia teknolojia kuhakikisha uzingatiaji sheria kuhusu ushuru.

Website | + posts