Mshambulizi wa Misri na klabu ya Liverpool Mohammed Salah,mshambulizi wa Nigeria na klabu ya Napoli Victor Osimhen, na beki wa Morocco na klabu ya PSG Achraf Hakimi wameteuliwa katika orodha ya wanandinga watatu wa mwisho wanaowania tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka huu Barani Afrika.
Mshindi atabainika Jumatatu usiku Disemba 11, wakati wa hafla za CAF za kuwatuza wanasoka bora ziotakazoandaliwa mjini Marrakech Morocco.
Tuzo ya mwanandinga bora wa mwaka kwa wanawake inawaniwa na mshindi wa mwaka jana Asisat Oshoala wa Nigeria na klabu Barcelona,Thembi Kgatlana wa Afrika Kusini na klabu ya Racing Louisville na Barbara Banda wa Zambia na klabu ya Shanghai Shengli.
Tuzo ya timu bora ya mwaka kwa wanaume inawindwa na Gambia,Morocco na Senegal huku ya wanawake ikiwaniwa na Morocco,Nigeria na Afrika Kusini.
Tuzo ya klabu bora ya mwaka kwa wanaume walio katika orodha ya mwisho ni Al Ahly ya Misri,Wydad Athletic ya Morocco na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini huku ya wanawake ikiwaniwa na AS FAR ya Morocco,Sporting Casablanca ya Morocco na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Tuzo nyingine zitakazowaniwa ni kipa bora wa mwaka kwa wanaume na wanawake,mchezaji chipukizi bora wa mwaka kwa wanaume na wanawake na mchezaji bora wa mwaka miongoni mwa wale wanaocheza soka barani Afrika.