Mwanamuziki wa Uganda wa mtindo wa Rap Gravity Omutujju amefafanua kiini cha uhusiano mbaya uliopo kati yake na mwanamuziki mwenza Bobi Wine ambaye pia ni kiongozi wa upinzani.
Kulingana naye, Bobi Wine alimkasirikia wakati wa kampeni mwaka 2017 akitafuta ubunge wa eneo la Kyadondo mashariki.
Omutujju anasema alialikwa kama mmoja wa watumbuizaji kwenye mkutano wa kampeni wa Bobi Wine katika eneo la Kiteezi na alipoomba pesa za kuweka gari mafuta Wine akakasirika.
Anasema Wine ambaye alidhania angetumbuiza bure bila malipo amemwekea kinyongo tangu wakati huo.
Gravity anasema hakuitisha malipo stahili kama ambayo huwa wanaitisha wakialikwa kwenye matamasha ila alitaka tu pesa za kufanikisha usafiri wake hadi eneo la tukio.
Mwaka jana Gravity alisema kwamba aliamua kufuta namba ya simu ya rafiki yake wa zamani Bobi Wine.
Amefafanua pia kwamba ugomvi wake na Wine haujafadhiliwa na serikali kwani yeye huwa haegemei upande wowote wa siasa nchini Uganda, akiongeza kusema kwamba anaweza kutumbuiza kwenye hafla ya chama cha Bobi Wine NUP iwapo ataalikwa na kulipwa.