Home Habari Kuu Gharama ya maisha haistahimiliki nchini, Azimio yaiambia serikali

Gharama ya maisha haistahimiliki nchini, Azimio yaiambia serikali

0

Muungano wa upinzani wa Azimio umekashifu hatua ya serikali kutangaza ongezeko kubwa la bei za mafuta nchini, ukitaja hatua hiyo kama itakayokuwa mzigo mkubwa kwa Wakenya ambao tayari wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.

Ukiongozwa na Raila Odinga, muungano huo sasa unatoa wito kwa Rais William Ruto kuingilia kati na kuwanusuru Wakenya dhidi ya makali ya gharama ya juu ya maisha kabla ya mambo kutumbukia nyongo zaidi.

“Jana, usiku wa manane, gharama ya mafuta ya dizeli ilipanda kwa shilingi 21. Bei ya mafuta taa iliongezeka kwa shilingi 33. Mafuta ya petroli yaliongezeka kwa shilingi 16. Huwezi ukasimamia uchumi kupitia propaganda. Mwaka mmoja baadaye, kila ishara inaashiria maisha yanadorora wala hayaimariki,” alisema Raila wakati akiwahutubia wanahabari leo Ijumaa akiandamana na viiongozi wengine wa Azimio.

“Bei ya kila bidhaa za msingi maishani zimeongezeka. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, bei ya kilo moja ya sukari imeongezeka kwa asilimia 61, ile ya kilo moja ya unga wa mahindi imeongezeka kwa asilimia 9.6, gharama ya chumba kimoja cha kukodi imepanda kwa asilimia 2.8 wakati kilowatt 50 za umeme zikipanda kwa asilimia 68.7,” aliongeza Raila wakati akitathmini utendakazi wa serikali ya Kenya Kwanza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Alinukuu bidhaa mbalimbali kuthibitisha madai yake kuwa bei ya bidhaa mbalimbali nchini imeongezeka kwa kipindi cha mwaka mmoja ambacho serikali ya Kenya Kwanza imekuwa mamlakani.

Raila akitumia fursa hiyo kutoa onyo kwa utawala wa Kenya Kwanza kuchukua hatua na kurekebisha hali ya mambo la sivyo ukabiliwe na hatima iliyokumba serikali zingine zilizozembea kazini kote barani Afrika.

Matamshi ya kinara huyo wa ODM yanakuja saa chache baada ya Halmashauri ya Kudhibiti Bei za Nishati na Mafuta, EPRA kutangaza bei mpya za mafuta jana Alhamisi usiku zilizoanza kutekelezwa mara moja.

Katika taarifa iliyotolewa na halmashauri hiyo, lita moja ya mafuta ya petroli jijini Nairobi kwa sasa inauzwa kwa shilingi 211.64 baada ya kuongezwa kwa shilingi 16.96, lita moja ya dizeli inauzwa kwa shilingi 200.99 baada ya kuongezwa kwa shilingi 21.32 wakati mafuta taa yakiuzwa kwa shilingi 202.61 kwa lita baada ya kuongezwa kwa shilingi 33.13.

Jijini Mombasa, mafuta ya petroli sasa yanauzwa kwa shilingi 208.58 kwa lita, dizeli shilingi 197.93 kwa lita wakati mafuta taa yakiuzwa kwa shilingi 199.54 kwa lita.

Jijini Kisumu, wakazi wamelazimika kuchomoa hela zaidi mifukoni na kununua mafuta ya petroli kwa shilingi 211.40 kwa lita wakati yale ya dizeli yakiuzwa kwa shilingi 201.16 kwa lita. Mafuta taa jijini humo yanauzwa kwa shilingi 202.77 kwa lita.

Mjini Kakamega, mafuta ya petroli yanauzwa kwa shilingi 211.45 kwa lita, dizeli shilingi 201.21 kwa lita huku mafuta taa yakiuzwa kwa shilingi 202.83 kwa lita.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa EPRA Daniel Bargoria, hatua ya halmashauri hiyo inatokana na ongezeko la kufikisha mafuta yaliyoagizwa nchini ambapo gharama za kusafirisha mafuta ya petroli hadi Mombasa ziliongezeka kwa asilimia 4.80, mafuta ya dizeli kwa asilimia 12.52 na mafuta taa kwa asilimia 19.79.

 

Website | + posts