Gavana wa kaunti ya Kiambu Kimani Wamatangi amefutilia mbali madeni ya matibabu yanayodaiwa wagonjwa 60 ya shilingi milioni 4 katika hospitali ya Thika Level 5.
Gavana huyo alitoa agizo la kuachiliwa kwa wagonjwa wote, baadhi yao wakiwa wamezuiliwa kwa muda wa zaidi ya miezi sita.
Wagonjwa 24 tayari wameruhusiwa kuondoka hospitalini.
Akizungumza wakati wa kuruhusu kundi la kwanza la wagonjwa kwenda nyumbani, meneja wa bodi ya kaunti hiyo Gathii Kanyi, alisisistiza kuwa wagonjwa waliozuiliwa hospitalini walisababisha msongamano wa wagonjwa hususan katika hospitali ya Thika level 5.
“Nawasihi wote walioruhusiwa kuondoka hospitalini, wajisajili na bima ya afya ya jamii SHA, na washiriki mpango wa afya wa kaunti ya Kiambu almaarufu Wamatangi Care,” alishauri Kanyi.
Alisema mpango huo mpya wa afya utawapumguzia wananchi mzigo wa gharama ya juu ya afya.