Home Kaunti Gavana Wamatangi afanyia mabadiliko kamati ya ukaguzi wa mji wa Thika

Gavana Wamatangi afanyia mabadiliko kamati ya ukaguzi wa mji wa Thika

0

Gavana wa kaunti ya Kiambu Kimani wa Wamatangi ameifanyia mabadiliko kamati ya kukagua na kutathimini uimarishaji wa mji wa Thika kuwa jiji.

Gavana Wamatangi amesema kuwa amebadilikisha wanachama wa awali na kuteua wapya kutoka sekta mbalimbali.

Aliyazungumza hayo wakati wa hafla moja huko Githunguri.

Wanachama walioteuliwa ni pamoja na Sylvia Mueni Kasanga wa muungano wa wasanifu mijengo, Gitu Kahengeri kutoka muungano wa wana sheria nchini na Zachary Nga’ng’a wa muungano wa miji na jiji.

Wengine ni Jeanter Warigia kutoka taasisi ya uhasibu wa umma, T.G.Ngorongo kutoka taasisi ya upangaji, Julius Macharia Chege atawakilisha taasisi ya masoroveya naye Cecilia Wamaitha atawakilisha muungano wa wafanyabiashara wa kaunti hiyo.

Vile vile, miji ya manispaa iliyoko karibu na mji wa Thika kama vile Juja, Gatundu, Githurai, Kabete na Githunguri itaboreshwa.

Hata hivyo, Thika inakabiliana na changamoto kadhaa zikiwemo ukosefu wa taa za barabarani, shida ya usafiri, sehemu za kuegesha magari, uhaba wa maji na mizozo ya shamba miongoni mwa zingine.

Kamati hiyo itapigwa msasa na bunge la kaunti hiyo kabla ya kuanza kazi.