Huku mjadala ukiendelea miongoni mwa wakenya kuhusu kubuniwa kwa kaunti tano mpya, Gavana wa kaunti ya Kitui Julius Malombe, ameunga mkono pendekezo hilo, ambapo anapigia debe kubuniwa kwa kaunti ya Mwingi.
Akizungumza siku ya Jumanne, Gavana Malombe alidokeza kuwa eneo la mwingi ambalo lina maeneo bunge matatu yanayojumuisha Mwingi Kaskazini, Mwingi ya kati na Mwingi Magharibi, linauwezo wa kuwa Kaunti.
Huku akilinganisha na maeneo mengine yaliyogatuliwa kama vile Lamu na Turkana, Malombe alisema Mwingi ina idadi kubwa ya watu kuliko kaunti hizo mbili.
Kulingana na ripoti ya idadi ya watu nchini ya mwaka 2019, idadi ya watu katika eneo la Mwingi ni 350,000, Lamu ikiwa na watu 143,000 nayo Samburu watu 310,000.
Aidha Malombe alitoa wito wa ushirikishi wa umma kikamilifu, kabla ya maamuzi ya mwisho kufanywa na bunge la kitaifa na lile la Seneti.