Home Kimataifa Gavana Sakaja atozwa faini ya nusu milioni na kamati moja ya Seneti

Gavana Sakaja atozwa faini ya nusu milioni na kamati moja ya Seneti

Sakaja alitakiwa kufika mbele ya kamati hiyo ili kujadili kuhusu mpango wa ukarabati wa mitaa ya zamani Jijini Nairobi.

0
kra

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, ametozwa faini ya shilingi 500,000 kwa kukaidi agizo la kufika mbele ya kamati ya Seneti kuhusu barabara, uchukuzi na nyumba kwa mara ya sita.

Kulingana na mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Seneta wa Kiambu Karungo Thangwa, Sakaja alialikwa kufika mbele ya kamati hiyo mara ya kwanza mnamo tarehe 30 mwezi Novemba mwaka 2022.

kra

Hata hivyo mwaka mmoja baadaye, hajawahi hudhuria mkutano hata mmoja wa kamati hiyo licha ya kualikwa na hatimaye kuagizwa.

“Natoa agizo kwa Gavana wa Nairobi kulipa faini ya shilingi 500,000 kutoka mfukoni make Wala asitoke fedha hizo kwa hazina ya kaunti ya Nairobi. Gavana huyo anapaswa kusitishwa safari zake za ughaibuni na kufika mbele ya kamati hiyo tarehe 30 mwezi  Novemba mwaka 2023 saa tano kamili bila kukosa,” aliagiza Thangwa.

“Gavana  Sakaja anapaswa kukabidhi kamati hiyo hati zake za kusafirisha, kama thibitisho alikuwa nje ya nchi,” aliongeza Seneta huyo

Sakaja alitakiwa kufika mbele ya kamati hiyo ili kujadili kuhusu mpango wa ukarabati wa mitaa ya zamani Jijini Nairobi.

Seneta wa Nairobi  Edwin Sifuna, alidokeza kuwa mipango yote ya ukarabati wa mitaa ya zamani ya Nairobi inapaswa kusitishwa hadi Gavana huyo afike binafsi mbele ya kamati hiyo.

Aliongeza kuwa ikiwa Gavana huyo atakosa kufika Alhamisi wiki hii, kamati hiyo itamuagiza Inspekta Jenerali wa polisi kumkamata na kumfikisha katika kamati hiyo.

Website | + posts