Home Kaunti Gavana Nyong’o aitaka serikali kutafakari upya kuhusu ushuru

Gavana Nyong’o aitaka serikali kutafakari upya kuhusu ushuru

0

Gavana wa kaunti ya kisumu Profesa Anyang Nyong’o ameitaka serikali kuu na bunge kujadili kuhusu ushuru inaotoza wananchi na kufanya marekebisho.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Ny’ongo alishangaa kwamba Wakenya wanatozwa kiwango kikubwa cha ushuru ambao wote utatumika kulipa madeni na wala sio wa kuwekeza.

“Tutajengaje utajiri, kuajiri wakenya na kuwatoza ushuru wa kiwango cha awali kwa sababu watakuwa wamejipatia kipato zaidi?” alishangaa Nyong’o.

Alihimiza serikali imsikilize Waziri Mkuu wa Uingereza ambaye amesifia Waziri wake wa Fedha kwa kupunguzia wananchi ushuru kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi, kujenga utajiri na kuhakikisha ajira kwa wananchi.

Gavana huyo aligusia kuhusu serikali yao ya NARC akisema kwamba walipoingia mamlakani mwaka 2002, waliamua kwamba mkakati wao wa ukuaji wa uchumi ni kukuza utajiri na kuhakikisha fursa za ajira.

“Tuliamua kwamba mkakati wetu kuhusu ushuru ungekuwa kupunguza ushuru na kuongeza idadi ya walipa ushuru,” alisema Nyong’o kwenye taarifa hiyo.

Kulingana naye, hiyo ndiyo njia pekee ya kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa hili.

Alielezea walifahamu fika kwamba serikali waliorithi haikuwa na pesa za kutosha lakini hawakutafuta mikopo ya kufadhili bajeti yao ya kwanza.

Baada ya mwaka mmoja, anasema uchumi ulikua kwa kiwango kikubwa na bajeti iliyofuata ikazidi trilioni moja.

Website | + posts