Home Habari Kuu Gavana Nassir: Kaunti hazijapokea fedha za kukabiliana na athari za El Nino

Gavana Nassir: Kaunti hazijapokea fedha za kukabiliana na athari za El Nino

0

Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir amekanusha madai kuwa kaunti zimepokea fedha za kukabiliana na athari za mvua ya El Nino inayoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini. 

Kaunti ya Mombasa ni miongoni mwa kaunti ambazo zimeathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua hizo na kusababisha wakazi wengi kuachwa bila makazi.

“Kumekuwa na madai kuwa serikali kuu imezikabidhi kaunti shilingi bilioni 10 za kukabiliana na athari za mvua ya El Niño. Ili kuondoa mashaka, licha ya changamoto, serikali ya kaunti ya Mombasa imekabiliana na athari za mvua hiyo ikitumia rasilimali zake yenyewe na kwa kusaidiwa na Shirika la Msalaba Mwekundu, mashirika yasiyokuwa ya serikali na taasisi huru kwa mantiki ya nia njema,” alisema Gavana Abdulswamad wakati akiwahutubia wanahabari.

“Bunge na Mdhibiti wa Bajeti wanapaswa kuchunguza madai haya ya usambazaji wa shilingi bilioni 10 na kuwabainisha raia ni wapi fedha hizi zilienda kwa sababu hazikupokelewa na kaunti.”

Gavana wa kaunti ya Siaya James Orengo aliyeandamana naye aliunga mkono msimamo huo.

Kauli za Gavana Abdulswamad zinafuatia hatua ya Naibu Rais Rigathi Gachagua jana Jumanne kuonekana kumnyoshea kidole cha lawama akimtaka kutumia fedha zilizotolewa na serikali kuu kwa serikali za kaunti kukabiliana na athari za mvua ya El Nino kwa kuwanunulia wakazi waliopoteza makazi chakula na bidhaa zingine muhimu.

Akiwagawia wakazi wa Kisauni chakula na bidhaa zingine za matumizi, Gachagua aliwasifia Magavana wa kaunti za Mandera na Wajir akisema hadi kufikia sasa, wametumia kitita cha shilingi milioni 50 kukabiliana na athari za mafuriko.

Kulingana naye, Gavana Abdulswamad anapaswa kuiga mfano wao.

Hali hiyo ya kulaumiana inajiri wakati Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini imetawaka Wakenya kujiandaa kwa mvua zaidi katika kipindi cha siku saba zijazo.