Home Habari Kuu Gavana Nassir apiga marufuku uuzaji na matumizi ya muguka Mombasa

Gavana Nassir apiga marufuku uuzaji na matumizi ya muguka Mombasa

0

Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Nassir amepiga marufuku uuzaji na utumiaji wa muguka na bidhaa zake katika kaunti hiyo.

Katika agizo lililotolewa leo Alhamisi, Nassir amesema kuwa hakuna gari lolote linalobeba muguka litaruhusiwa kuinga kaunti hiyo ya eneo la Pwani.

Nassir pia aliagiza maduka yote yawe ya reja reja au ya jumla au ya kusambaza bidhaa hizo kufungwa mara moja.

“Idara za kaunti zimeagizwa kutekeleza agizo hili bila ubaguzi,” alisema Gavana huyo.

Gavana huyo alisema kuwa alichukua uamuzi huo baada ya kushauriana na Mamlaka ya Kitaifa ya Kampeni ya Matumizi ya Dawa za Kulevya (Nacada).

Aliongeza kwamba matumizi ya kisayansi ya muguka yamethibitisha kuwa yalisababisha ugonjwa wa afya ya akili na ulemavu.

“Husababisha madhara ya kiafya, kijamii, kiuchumi na kimazingira na kuweka mizigo kwa watoto, familia, maskini na mifumo ya afya ya kaunti,” alisema.

Gavana huyo ni miongoni mwa viongozi wa eneo la Pwani ambao wamekuwa mstari wa mbele wakipinga matumizi ya muguka.

Siku chache zilizopita, gavana huyo akizungumza katika shule moja ya msingi kaunti hiyo alipiga marufuku uuzaji wa muguka na miraa karibu na shule za umma.

Mnamo Jumatano wiki hii gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro alitangaza kupiga marufuku kabisa uuzaji wa muguka katika kaunti yake, akisema kuwa imekuwa tatizo kubwa kwa watoto.

Gavana Mung’aro alisema inasikitisha kushuhudia watoto wa umri wa miaka 10 wakila muguka, akitaja kuwa tishio kwa kizazi cha vijana.

Alphas Lagat
+ posts