Home Vipindi Gavana Mwangaza azindua mpango wa kugawia jamii maskini ng’ombe

Gavana Mwangaza azindua mpango wa kugawia jamii maskini ng’ombe

Gavana Mwangaza na baadhi ya walionufaika na mpango wa ng'ombe wa maziwa

Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza leo amezindua mpango wa kugawia jamii maskini ng’ombe kwa jina “One Dairy Cow, One Needy Family Program”.

Akizungumza katika eneo la Akithii huko Tigania Magharibi wakati wa uzinduzi huo, Gavana Mwangaza alisema mpango huo ni wa serikali ya kaunti ya Meru ambao uliratibishwa kupitia sera inayolenga kukuza ufugaju wa ng’ombe wa maziwa ya mwaka 2023.

Alisema sera hiyo ambayo iliidhinishwa na kamati kuu ya serikali ya kaunti ya Meru, ina mbinu bayana ya kutambua walengwa wa mpango huo kupitia kwa kamati za wadi mbali mbali.

Mwangaza aliongeza kusema kwamba katika mwaka huu wa kifedha ambao ni 2022/2023 wametenga shilingi milioni 50 za kununua ng’ombe hao na katika uzinduzi tayari wametumia milioni 17.

Kiongozi huyo alisema wanalenga kugawa ng’ombe 5000 kufikia mwaka 2027.

Alielezea kwamba kila ng’ombe anatolewa na banda lake na leo waligawa ng’ombe 10 na mabanda kumi.

Kufikia Juni 2024, Gavana mwangaza alisema watakuwa wamegawa ng’ombe 335 na idadi sawia ya mabanda ya ng’ombe kwa lengo la kuimarisha lishe bora na upatikanaji wa chakula kando na kuimarisha mapato ya familia husika.

Mpango huo alisema unatekelezwa kupitia kwa kurugenzi inayohusika na uimarishaji wa mifugo na ufugaji wa samaki ili kuhakikisha usimamizi bora wa fedha na uwajibikaji.

Mpango huo anasema unalenga kuongeza kiwango cha maziwa na matumizi ya maziwa akisema kiwango cha maziwa yanayokamuliwa kila siku katika kaunti ya Meru ni lita laki 8 na wanadhamiria kufikisha lita milioni moja kila siku.

Uzinduzi huu unajiri siku chache baada ya waziri wa mambo ya ndani Kithure Kindiki kupiga marufuku mikutano ya Gavana Mwangaza ya mpango wake wa “Okolea” baada ya mkutano wake mmoja kukumbwa na ghasia.

Website | + posts
Jeff Mwangi
+ posts