Home Kaunti Gavana Mung’aro apongeza juhudi za kukamilisha uhamisho wa majukumu na mali kwa...

Gavana Mung’aro apongeza juhudi za kukamilisha uhamisho wa majukumu na mali kwa magatuzi

Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro amepongeza juhudi za kamati ya kiufundi ya uhusiano kati ya serikali kuu na serikali za kaunti IGRTC, za kutekeleza azimio la awamu ya 10 ya kongamano la serikali hizo.

Azimio hilo linahusu kukamilisha uhamisho wa majukumu na mali kwa serikali za magatuzi mpango uliokwama kwa zaidi ya miaka 10 wakati ugatuzi umetekelezwa nchini.

Kaunti ya Kilifi ndiyo ya kwanza kupokea ripoti kuhusu tathmini ya ardhi na magari hatua ambayo Mung’aro anasema itawezesha serikali ya kaunti kulainisha orodha ya mali zake na kulinda mali ambayo imekuwa ikivutia wanyakuzi wa ardhi.

Kaunti ya Kilifi ina vipande vya ardhi 1,228 ambavyo umiliki wake unastahili kuhamishiwa serikali ya kaunti na vingi kati ya vipande hivyo vimeingiliwa na wanyakuzi na maskwota.

Mung’aro hata hivyo amesema inasikitisha kwamba baadhi ya magari ya serikali hayapo kwenye orodha ya magari yanayomilikiwa na serikali hata wakati wa mchakato wa hivi maajuzi wa utathmini.

Mkurugenzi mtendaji wa IGRTC Kipkurui Chepkwony anasema kwamba kamati hiyo pamoja na idara ya ugatuzi ya serikali kuu zinakamilisha utathmini na uhamisho wa mali za serikali mbali mbali za magatuzi pamoja na majukumu yaliyogatuliwa.

Haya ni kulingana na azimio la kongamano la kumi linalolenga kuboresha ugatuzi na utoaji huduma mashinani.

Serikali ya kaunti ya Kilifi imepokezwa mali zipatazo 259, nyingi zikiwa magari ambayo thamani yake ni takriban shilingi milioni 51 chini ya mpango ulioanzishwa na mamlaka ya mpito.

Lengo la mchakato mzima ni kusuluhisha maswali ya ukaguzi yanayotokana na fedha zinazotumiwa kwa magari ambayo hayapo kwenye sajili ya mali za kaunti.

Chepkwony alisema pia kwamba uhusiano mwema kati ya serikali kuu na serikali za kaunti kupitia mawasiliano na ushirikiano umekuwa nguzo katika kuhakikisha ugatuzi unanufaisha wakenya.

Website | + posts
Dickson Wekesa
+ posts