Home Kimataifa Gavana Mung’aro ampigia debe Hassan Joho kuwa kinara wa ODM

Gavana Mung’aro ampigia debe Hassan Joho kuwa kinara wa ODM

Gavana huyo wa Kilifi alisema kuwa ataongoza mchakato wa kuwasihi magavana wa eneo la Pwani kuunga mkono na kumuidhinisha Joho kuwa kinara wa ODM.

0
Gavana wa Kilifi Gideon Mung'aro.
kra

Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro, ametoa wito kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga, kumwachia Ali Hassan Joho kumrithi kama kinara wa chama cha Orange Democratic Movement,ODM.

Mung’aro alisema kuwa Gavana huyo wa zamani wa Mombasa, amekuwa mwaminifu katika chama hicho na kinara wake Odinga, na hivyo basi ni wakati wa mwanasiasa huyo kutoka Pwani kuongoza chama hicho maarufu nchini Kenya.

kra

“Wakazi wa Pwani wamekuwa waaminifu sana kwa chama cha ODM na kinara wa chama chetu Raila Odinga, na sasa ni wakati wa sisi kuchukua uongozi huku Raila akielekea AUC. Raila angali kiongozi wetu wa chama hadi wakati kama huo atatangaza vinginevyo na wakati huo ukifika, Joho ndiye atakayesimamia chama,” alisema Mung’aro.

Kampeni za kumrithi Raila iwapo atachaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika (AUC) zimechacha baina ya Joho na aliyekuwa gavana wa kaunti ya Kakamega Wycliff Oparanya. Wawili hao ni manaibu wa Raila katika chama cha ODM.

Gavana huyo wa Kilifi alisema kuwa ataongoza mchakato wa kuwasihi magavana wa eneo la Pwani kuunga mkono na kumuidhinisha Joho kuwa kinara wa ODM.

“Kama mwenyekiti wa magavana wa Pwani, nitawakusanya magavana wote wakiwemo wa vyama vingine kuzungumza kwa sauti moja na kumuunga mkono Joho kuwa kiongozi wa chama cha ODM,” alisema gavana huyo.

Alphas Lagat
+ posts