Home Habari Kuu Gavana Lenku atozwa faini kwa kukosa kufika Seneti

Gavana Lenku atozwa faini kwa kukosa kufika Seneti

0

Gavana wa kaunti ya Kajiado Joseph ole Lenku ametozwa faini ya shilingi laki 5 na kamati ya bunge la Seneti kuhusu barabara na usafiri.

Hii ni baada ya Gavana Lenku kukosa kufika mbele ya kamati hiyo.

Alitarajiwa kujibu maswali kuhusu upatikanaji wa hatimiliki za ardhi za Jamii Bora Estate iliyoko Kisaju katika kaunti ya Kajiado.

Seneta wa kaunti ya Kiambu Karungo Thang’wa ni mwenyekiti wa kamati ya bunge la Seneti kuhusu barabara na usafiri. Alielezea kwamba walilazimika kuchukua hatua hiyo kwa sababu walitoa mwaliko kwa Gavana Lenku kwa wakati na hakuashiria kwamba hangeweza kufika hadi leo.

“Tulimwandikia Gavana mara kadhaa tukimwomba atoe taarifa hitajika, tukaandika nyaraka za ukumbusho kwake lakini hakuridhia, kamati ikaamua kumwalika kwa kikao hiki,” alisema Thang’wa.

Aliongeza kwamba walipokea mawasiliano ya simu leo dakika 45 kabla ya mkutano kuwafahamisha kwamba Gavana Lenku hangeweza kufika.

Watu kadhaa walioathirika na upatikanaji wa hati hizo za umiliki wa ardhi walifika katika eneo la kikao cha leo wakitarajia kupata maelezo ya Gavana Lenku lakini hayo hayakutimia.

Utata kuhusu vipande hivyo vya ardhi unatokana na hatua ya Jamii Bora Trust kuamua kubadilisha matumizi ya ardhi hiyo.

Walipoinunua walisema kwamba ingetumika kujenga nyumba za makazi ambako watu kutoka mitaa ya mabanda jijini Nairobi wangehamia.

Baadaye, wakabadili nia na kuigawanya ardhi hiyo katika vipande vidogo na kuuzia watu binafsi, hatua ambayo sasa ilihitaji walipe ushuru kwa serikali ya kaunti.

Ushuru ambao Jamii Bora Trust inadaiwa ndio umesababisha hatimiliki za awali mbili zikose kubadilishwa na kuwa hatimiliki 5,871.

Website | + posts