Home Habari Kuu Gavana Kawira Mwangaza wa Meru ajiunga na UDA

Gavana Kawira Mwangaza wa Meru ajiunga na UDA

0

Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza amejiunga na chama cha UDA.

Mwangaza alifika katika makao makuu ya chama hicho jijini Nairobi leo Jumatano na kutangaza kujiunga na chama hicho kinachoongozwa na Rais William Ruto.

Alipokelewa na mwenyekiti wa chama cha UDA Cecily Mbarire na Katibu Mkuu Cleophas Malalah.

“Nimefurahi kuwaonyesha wakazi wa Meru njia, chama ni UDA,” alisema Mwangaza aliyegombea ugavana wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022 kama mgombea huru.

Kwa kujiunga na UDA, Gavana Mwangaza anatarajiwa kutetea wadhifa wake kwa tiketi ya chama hicho katika hatua ambayo huenda ikabadilisha dira ya kisiasa ya kaunti ya Meru.

Gavana huyo kwa muda mrefu amekuwa akihasamiana na viongozi wengi wa eneo la Meru, wengi wao ambao ni wanachama wa UDA.

Uhasama kati yao ulisababisha bunge la kaunti linalotawaliwa na wawakilishi wadi wengi wa UDA kujaribu kumtimua mamlakani ingawa jitihada zao mara mbili zilizimwa na bunge la Seneti.

Kwa kujiunga na UDA, haijulikani ikiwa hatua hiyo itasaidia kukuza uhusiano mwema kati ya Gavana Mwangaza na mahasimu wake wa kisiasa.

Website | + posts