Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza, amepongeza bunge la Seneti kwa kumnusuru baada ya kutupilia mbali mashtaka yote saba dhidi yake jana Jumatano usiku.
Kupitia kwenye ukurasa wake wa X, Gavana Mwangaza alimshukuru Mungu kwa ushindi na kusema, “kaunti ya Meru imeibuka na ushindi.”
Gavana huyo alibubujikwa na machozi punde baada ya kusomwa kwa matokeo ya kura na uamuzi wa Maseneta hiyo jana.
Ilikuwa ni mara ya pili kwa Gavana Mwangaza kuokolewa na Seneti, baada ya kuondolewa mashtaka tena mwezi Disemba mwaka uliopita.
Hata hivyo, mtihani mkubwa unaomkabili kwa sasa ni jinsi atakavyotekeleza majukumu yake na ushirikiano wake na wawakilishi wadi wa kaunti hiyo ambao amekuwa akivutana nao mara kwa mara.