Home Habari Kuu Gavana Kawira aona Mwangaza tena baada ya Seneti kumnusuru

Gavana Kawira aona Mwangaza tena baada ya Seneti kumnusuru

0

Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza, aliponea chupuchupu kung’atuliwa afisini kwa mara ya pili, baada ya Maseneta jana Jumatano usiku kutupilia mbali mashtaka yote saba yaliyowasilishwa dhidi yake na bunge la kaunti hiyo.

Maseneta 28 walipiga kura kupinga kosa la ubadhirifu wa pesa, wakisema alikuwa hana hatia huku Maseneta 19 wakisema alikuwa na hatia.

Maseneta 42 walipiga kura kupinga kosa la mashtaka ya Gavana huyo kuwa mwenye mapendeleo ya kikabila katika uajiri na matumizi mabaya ya afisi huku watano wakimhukumu.

Katika kosa la tatu la kuwakandamiza watu na kuwadunisha viongozi wengine, Maseneta 44 walipiga kura ya kupinga na watatu pekee wakaunga mkono.

Kosa la nne dhidi yake la uteuzi usiofuata sheria na kukiuka mamlaka yake, Maseneta 26 walipinga na wengine 20 wakaunga mkono.

Maseta 44 walimwondolea Gavana kosa la kudharau mahakama na watatu wakamhukumu.

Kosa la sita la kuipa barabara jina la mumewe, Maseneta 43 walitupilia mbali na wengine wanne wakawaunga mkono wawakilishi wadi.

Maseneta 35 walipinga kosa la Gavana huyo kudharau bunge la kaunti ya Meru, huku wengine 10 wakiunga mkono wakisema alikuwa na hatia.

Kulingana na Spika wa bunge la Seneti Amason Kingi, Gavana Mwangaza atasalia afisini baada ya kuondolewa mashtaka yote dhidi yake.

Awali, wawakilishi wadi 59 walipiga kura kumng’atua mamlakani na uamuzi uliafikiwa baada ya mashtaka dhidi yake kusikizwa kwa siku mbili na Seneti.

Website | + posts