Home Kaunti Gavana Irungu ahofu juu ya maambukizi ya UKIMWI Laikipia

Gavana Irungu ahofu juu ya maambukizi ya UKIMWI Laikipia

0
Gavana wa Laikipia Joshua Irungu
Gavana wa Laikipia Joshua Irungu
Gavana wa Laikipia Joshua Irungu amefanya mkutano wa ushauriano na wataalam wa afya wakiongozwa na USAID TUJENGE JAMII ili kuangazia changamoto za afya zinazoikumba kaunti hiyo.  
Akiwahutubia wataalam hao, Irungu amesema inakatisha tamaa kwa kaunti hiyo kuanza kurekodi visa vya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kutoka kwa mama hadi kwa mtoto wakati wa kujifungua licha ya juhudi zilizowekwa na kaunti kuikabili hali hiyo.
Gavana huyo sasa anatoa wito kwa washikadau wote kuungana na kufanya kazi kwa bidii ya mchwa kukabiliana na hali hiyo inayochipuka tena.
Amesema utawala wake umeweka mikakati mwafaka ya kuhakikisha hakuna maambukizi yoyote ya ugonjwa wa UKIMWI yanayoripotiwa kutoka kwa mama hadi kwa mtoto wakati wa kujifungua.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya wa kaunti hiyo amesema watatoa mafunzo kwa viongozi kutoka sekta zote kuhusiana na masuala ya afya kama njia ya kuhakikisha kaunti hiyo inatambuliwa kama iliyo na watu wenye afya nzuri.
Dkt. Moses Kitheka ambaye ni Mkuu wa pande zilizo chini ya mwavuli wa USAID TUJENGE JAMII aliishukuru serikali ya kaunti kwa juhudi zake za kukabiliana na changamoto katika sekta ya afya zinazohusiana na virusi vya HIV na UKIMWI akisema hatua hiyo itasaidia sekta ya afya kuimarisha afya ambayo ni moja ya nguzo ya kuhakikisha upatikanaji wa jamii inayostawi.
Lydia Mwangi
+ posts