Home Habari Kuu Gavana Abdullswamad Sheriff Nassir afanywa mzee wa jamii ya Luo

Gavana Abdullswamad Sheriff Nassir afanywa mzee wa jamii ya Luo

0
Gavana Nassir akivishwa kofia ya mzee wa jamii ya Luo

Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdullswamad Sheriff Nassir alitawazwa kuwa mzee wa jamii ya Luo katika hafla iliyofanyika kwenye uwanja wa maonyesho wa Mkomani huko Mombasa kwenye tamasha ya kitamaduni ya jamii ya Luo.

Nassir ambaye alipatiwa jina la “Omondi Jabondo” alivishwa mavazi kamili ya mzee wa jamii ya Luo pamoja na ngao na mkuki.

Akizungumza baada ya kutawazwa, Gavana huyo alishukuru kwa utambuzi huo kama mzee wa jamii ya Luo na akaahidi kuunganisha watu wote wanaoishi katika kaunti ya Mombasa bila kujali misingi ya kabila.

Alimshukuru Ker Odungi Randa ambaye aliongoza shughuli hiyo na ambaye pia alitambuliwa na baraza la wazee wa jamii za Mijikenda Kaya.

Kulingana naye, hatua hiyo inalenga kuwianisha jamii za eneo hilo.

Wanaofanya kazi katika afisi ya Gavana wa Mombasa wa asili ya Luo walimtunuku Nassir zawadi ya ng’ombe ambayo alikabidhiwa na kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga.

Alihimiza waandalizi wa tamasha hiyo waifanye iwe ya kila mwaka.

Shughuli hiyo ilihudhuriwa na viongozi wengi akiwemo kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua na kiongozi wa wachache bungeni Opiyo Wandayi.

Mwanamuziki Prince Indah alitumbuiza kwenye hafla hiyo.