Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi ametoa wito kwa Wakenya kutofuata njia haribifu ya nchi kama vile Somalia na Sudan.
Ameonya dhidi ya vitendo ambavyo vinaweza vikaisambaratisha nchi hii.
Huku akikiri kuwa kila mtu ana haki ya kuandamana na kuwasilisha malalamiko kwa mamlaka kwa njia ya amani na bila silaha, Gavana Abdullahi amelalamika kwamba maandamano ya amani yaliyoitishwa na vijana wa Gen Z yanaelekea njia ya machafuko.
Amesisitiza haja ya kuwepo mazungumzo ya amani na uwazi ili kuangazia changamoto zinazoikumba nchi, akionya dhidi ya utumiaji wa njia zisizokuwa za kikatiba kumtimua Rais madarakani.
Aliyasema hayo mjini Meygag, Wajir Kusini katika kaunti ya Wajir wakati wa uzinduzi wa mradi wa usambazaji wa umeme vijijini wa Meygag.
“Kuna hashtagi ambayo kwa sasa imeenea baada ya Mswada wa Fedha kuondolewa na Rais mwenyewe kukataa kuutia saini na kuurejesha bungeni. Sasa, watu wengi wanasema Rais anapaswa kuondolewa. Wale wanaosema hivyo hawafahamu wanachokiombea. Rais hawezi akaondolewa kwa njia zisizokuwa za kikatiba,” amesema Abdullahi.
“Hiyo itakuwa sawa na kuichoma nchi hii, na sina uhakika hicho ndicho wanachokitaka vijana wa Gen Z.”
Rais Ruto ameelezea nia ya kushiriki mazungumzo na vijana hao wanaofanya maandamano nchini ili kusikiliza na kuangazia masuala yanayowatia tumbo joto.
“Kama Gavana wa kaunti katika jamhuri yetu ambaye anashirikishana mpaka mrefu zaidi na Somalia, nafahamu kwamba uharibifu unahitaji jitihada ndogo. Kujenga taifa na kuliunganisha si rahisi, na hatutaki kwenda njia sawa na mataifa ya Somalia na Sudan.”