Home Habari Kuu Gachagua: Serikali itatumia rasilimali zote kukabiliana na athari za El Nino

Gachagua: Serikali itatumia rasilimali zote kukabiliana na athari za El Nino

Idara ya utabiri wa hali ya hewa, ilidokeza kuwa mvua ya El Nino itaanza mwezi Oktoba na kufululiza hadi mwezi Januari mwakani

0
Naibu Rais Rigathi Gachagua andaa mkutano wa kukabiliana na majanga ya El Nino.

Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema serikali itahakikisha idara zake zote zimejiandaa vilivyo kukabiliana na athari zozote za mvua ya El Nino.

“Ninatoa hakikisho kwamba serikali itatumia rasilimali zote zilizopo kukabiliana na changamoto za mvua ya El Nino,”alisema Gachagua.

Gachagua alidokeza kuwa serikali inajizatiti kuzuia majanga kutokea, badala ya kusubiri majanga hayo kutokea wakati wa mvua hizo,hii ni kupitia mipangilio bora na ushirikiano na wadau tofauti.

“Kukosa kujipanga, ni kupanga kufeli. Tulete mawazo yetu pamoja ili tuepuke kushughulika majanga yanapotokea ambayo yanaweza kuzuiwa,”alidokeza naibu huyo wa Rais.

Alitoa wito kwa serikali za kaunti kushirikiana na ile ya kitaifa katika juhudi za kuzuia kutokea majanga wakati wa msimu wa mvua ya El Nino.

“Serikali hizo mbili hazina ushindani wowote. Serikali za kaunti zishirikiane na ile ya kitaifa kwa mipangilio bora,” aliongeza Gachagua.

Naibu huyo wa Rais aliyasema hayo Alhamisi alipokutana na mawaziri husika, Magavana, makundi ya kushughulikia dharura na washirika wa kimataifa, kujadili mbinu za kuzuia majanga wakati wa msimu wa mvua za El Nino.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa, ilidokeza kuwa mvua ya El Nino itaanza mwezi Oktoba na kufululiza hadi mwezi Januari mwakani.