Naibu rais Rigathi Gachagua amesema serikali inaratibu mfumo wa kwaunganisha wafanayakazi katika sekta ya jua kali walioidhinishwa na fursa za ufadhili wa kibiashara humu nchini na kimataifa.
Naibu rais amesema mfumo huo utatoa mwelekeo wa mpito wa nguvu kazi kutoka sekta ya jua kali hadi fursa nyingine za kibiashara zenye malipo bora,kwa lengo la kuwawezesha kuchangia kikamilifu kwa ukuzi wa uchumi wa taifa hili.
Akizungumuza wakati wa mkutano wa wadau mbali mbali katika makazi yake rasmi ya Karen, jijini Nairobi, naibu rais alitaja uamuzi wa kuunganisha sekta ya jua kali na vyuo vya mafunzo ya kiufundi kuwa mpango mahususi wenye manufaa makubwa kwa ukuzi wa uchumi.
Aidha naibu rais alisema mpango huo pia utaongeza ushiriki wa mafundi wa jua kali katika mradi wa serikali wa ujenzi wa nyumba za gharama nafu na masoko.
Afisa mkuu mtendaji wa shirikisho la mafundi wa jua kali Nyamai Wambua aliishukuru serikali kwa mpango huo akisema utafungua nafasi za ajira kwa watu wanaofanya kazi katika sekta ya jua kali.
Matamshi yake yaliungwa mkono katibu wa maswala ya ughaibuni Roseline Njogu ambaye alisema mafundi wa jua kali walioidhinishwa watajumuishwa kwenye mpango wa ajira ugenini almaarufu Kazi Majuu .