Home Kaunti Gachagua: Serikali inajizatiti kuhakikisha wakulima wa miraa wananufaika

Gachagua: Serikali inajizatiti kuhakikisha wakulima wa miraa wananufaika

0

Naibu rais Rigathi Gachagua amewahakikishia wakulima wa Miraa usaidizi wa serikali, ili wajinufaishe na mmea huo na hivyo kuinua maisha yao.

Akizungumza Ijumaa akiwa katika eneo la Tigania kaunti ya Meru, naibu huyo wa rais alisema miraa ni kipato pekee kwa familia nyingi, na kwa sababu hiyo, aliahidi ushirikiano na wadau wengine kuhakikisha mmea huo unaondolewa kwenye orodha ya madawa ya kulevya.

Aidha, alisema serikali ya Kenya Kwanza imemakinika na mabadiliko katika sekta ya Kilimo kwa lengo la kuinua wakulima.

“Majuma matatu yaliyopita tuliandaa mkutano kujadili kahawa hapa Meru. Tunajizatiti kuimarisha wakulima wa miraa. Tutawachagua wakulima wachache kutoka Meru kuelekea katika nchi za nje ili kutafuta soko la mmea huo,” alisema naibu huyo wa rais.

Mamlaka ya kitaifa ya kampeni dhidi ya mihadarati NACADA imeorodhesha miraa kama mihadarati, hatua ambayo imepingwa vikali.

Wakati wa mkutano katika kaunti ya Meru, naibu rais alitoa hundi ya shilingi milioni tano kwa shule ya upili ya wasichana ya Kianjai eneo bunge la Tigania magharibi kufadhili ujenzi wa ofisi za shule hiyo kama ilivyoahidiwa na rais William Ruto.

Naibu wa Rais alikuwa ameandamana na waziri wa kilimo Mithika  Linturi, waziri wa vyama vya ushirika Simon Chelugui, Gavana wa Meru Kawira Mwangaza na mwakilishi wanawake Elizabeth Karamu, miongoni mwa viongozi wengine.

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here