Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa hakikisho kwamba serikali imejitolea kuboresha sekta ya afya.
Akizungumza wakati wa sherehe ya 92 ya kufuzu ya taasisi ya kozi za afya nchini KMTC, naibu Rais aliangazia jukumu muhimu la wafanyakazi wa sekta ya afya walio na ujuzi katika kuafikia mpango wa huduma bora za afya kwa wote.
Matamshi ya naibu Rais yanawiana na lengo la kitaifa la kuhakikisha huduma bora za afya kwa wote bila kuwasababishia matatizo ya kifedha.
Alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika watendakazi walio na ujuzi akisema serikali itahakikisha watendakazi hao Wana ujuzi na vifaa hitajika ili waweze kutoa huduma bora za afya kwa wakenya wote.
Waziri wa afya Susan Nakhumicha Wafula kwa upande wake alisisitiza kujitolea kwa serikali kusaidia taasisi hiyo ili iendelee kutambuliwa kama taasisi Bora ya mafunzo ya afya.
Alitaka ziwepo juhudi za ushirikiano Ili kuhakikisha uendelevu katika mfumo wa elimu ya afya na huduma za afya.
“Yeyote anayekutana na mhudumu wa afya nchini au nje, huenda akatagusana na mtu aliyefuzu kutoka KMTC. Ninajivunia kuwa mwanafunzi wa zamani wa taasisi hii.” Alisema waziri Nakhumicha.
Aliongeza kwamba yeye ni mfano bora kwamba unaweza kuanzia katika taasisi ya KMTC na kukua hadi kiwango cha juu kabisa katika taaluma hiyo.
Kulingana na waziri huyo serikali inalenga kuimarisha miundomsingi ya afya kwa kuahidi kusaidia katika makuzi ya wafanyakazi wa sekta hiyo.
Karibu wa afya ya umma Mary Muthoni, ambaye pia alihudhuria sherehe hiyo alipongeza taasisi ya KMTC kwa kutoa watendakazi bora wa sekta ya afya walio tayari kuziba mianya iliyopo katika sekta hiyo.
Jumla ya wanafunzi 22,691 walifuzu leo.