Home Habari Kuu Gachagua: Ni haki ya Rais kulifanyia mabadiliko Baraza la Mawaziri

Gachagua: Ni haki ya Rais kulifanyia mabadiliko Baraza la Mawaziri

0
Naibu Rais Rigathi Gachagua
Naibu Rais Rigathi Gachagua

Rais William Ruto ana haki ya kulifanyia mabadiliko Baraza lake la Mawaziri. 

Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema mabadiliko yaliyofanywa juzi Jumatano yalikusudia kuboresha utoaji huduma kwa Wakenya.

“Hakuna aliyeondolewa ofisini. Hakuna haja ya kukisia mengi kuhusiana na mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais,” alisema Gachagua kupitia mtandao wake wa X leo Ijumaa.

“Tafadhali, nawaomba wale waliopewa majukumu mapya kufanya kazi kwa kumakinika na kujitolea na kuhakikisha kazi yao inaonekana machoni pa umma.”

Kauli zake zikiwadia wakati kumekuwa na makisio kuwa huenda alichangia kufanywa kwa mabadiliko hayo hususan kuhamishwa kwa Moses Kuria kutoka kwa Wizara ya Biashara hadi ile ya Utumishi wa Umma.

Katika siku za hivi karibuni, wawili hao wamedaiwa kuwa na tofauti za kisiasa, madai ambayo Gachagua ameyapuuzilia mbali.

Katika mabadiliko hayo, Musalia Mudavadi aliongezwa majukumu na sasa atahudumu kama Waziri Mwenye Mamlaka Makuu na pia Waziri wa Mambo ya Nje.

Kabla ya mabadiliko hayo, Dkt. Alfred Mutua alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje.

Dkt. Mutua sasa atahudumu kama Waziri wa Utalii na Wanyama Pori, wadhifa ambao ulishikiliwa na Peninah Malonza.

Malonza sasa ametwikwa jukumu la kuongoza Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Maeneo Kame na Maendeleo ya Kikanda ambayo awali ilishikiliwa na Rebeccah Miano.

Miano sasa ndiye Waziri mpya wa Biashara, akijaza pengo lililoachwa na Kuria.

Aisha Jumwa sasa atahudumu kama Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi.

Waziri wa Maji Alice Wahome ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akilumbana na Katibu katika wizara hiyo pia amehamishwa katika mabadiliko hayo.

Wahome sasa ameteuliwa kuhudumu kama Waziri wa Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Ustawi wa Miji akibadilishana na Zacharia Njeru ambaye amateuliwa kumrithi katika Wizara ya Maji, Usafi na Unyunyiziaji Maji Mashamba.