Home Habari Kuu Gachagua: Kaunti 19 zimeathiriwa na mafuriko hapa nchini

Gachagua: Kaunti 19 zimeathiriwa na mafuriko hapa nchini

Ili kupunguza madhara ya mvua, naibu huyo wa Rais alisema serikali imepeleka ndege za jeshi kusaidia kuhamisha familia katika maeneo salama.

0
Naibu Rais Rigathi Gachagua ahutubia taifa kuhusu hali ya mvua hapa nchini.

Zaidi ya kaunti 19 katika maeneo kame hapa nchini zimeathiriwa na mafuriko kutokana mvua kubwa inayoshuhudiwa kote nchini.

Akihutubia wakenya siku ya Ijumaa, naibu Rais Rigathi Gachagua, alisema mafuriko yamesababisha maelfu ya familia kuhama makwao, huku mali ikiharibiwa, hasaa katika kaunti za  Garissa, Mandera, Wajir na Busia.

“Tunatambua kuwa mvua inayoendelea kunyesha katika sehemu nyingi za nchi imehatarisha maisha, lakini tunaweka mikakati ya kuwasaidia wale ambao wameathirika,” alisema naibu huyo wa Rais.

Gachagua alitoa wito kwa serikali ya kitaifa, zile za kaunti na taasisi zingine, kufanya kazi kwa karibu na mashirika ya kibinadamu kutoa rasilimali za kukabiliana na madhara yaliyosababishwa na  mvua.

“Kwa sasa serikali inasambaza mitihani ya kidato cha nne KCSE katika maeneo ambako barabara hazipitiki kutokana na mafuriko, vile vile serikali inapeleka chakula na bidhaa zingine za msingi kwa walioathiriwa, ili kuwapunguzia mateso,” aliongeza Gachagua.

Aidha ili kupunguza madhara ya mvua, naibu huyo wa Rais alisema serikali imepeleka ndege za jeshi kusaidia kuhamisha familia katika maeneo salama.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa ilisema taifa hili litashuhudia mvua kubwa kati ya mwezi Oktoba mwaka 2023 hadi mwezi Januari 2024.

Website | + posts