Naibu Rais Rigathi Gachagua, amewaonya viongozi dhidi ya kueneza siasa za migawanyiko, badala yake aliwahimiza kuwahudumia wananchi.
Akiwahutubia wakazi Nyeri mjini, baada ya kufungua rasmi maonyesho ya kilimo ya kaunti ya Nyeri, Gachagua aliwasuta baadhi ya viongozi aliodai wanajihusisha na kampeni za mapema na kuwagawanya wakenya kwa makundi ya kisiasa na kimaeneo.
Naibu huyo wa Rais alitoa wito kwa wakenya kupigia darubini utendakazi wa viongozi wao, na kuwapiga kumbo wale ambao wametelekeza majuku yao na kujihusisha na siasa za mapema.
Mimi siungi mkono siasa, napigia debe utendakazi. Ninamwelekeo na ninawahudumia wakenya. Msikubali siasa za migawanyiko, lakini mpigie kurunzi utendakazi wao,” alisema Gachagua.
Viongozi walioandamana na Gachagua walitoa wito wa kuheshimiwa kwa naibu huyo wa Rais, wakati huo huo wakiwashutumu wenzao kwa ujihusisha katika kampeni za mapema.
Wakiongozwa na Gavana wa kaunti ya Nyeri Mutahi Kahiga na Seneta wa Nyandarua John Methu, viongozi hao walisema wanaunga mkono serikali jumuishi iliyobuniwa na Rais William Ruto.
“Sisi kutoka Mlima Kenya tunamtambua naibu wa Rais kuwa kiongozi wetu wa kisiasa. Tuna wasiwasi kwa sababu badala ya viongozi kuwahudumia wakenya, wanajihusisha na siasa za mapema,” alisema Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga.
Viongozi hao ni pamoja na wabunge James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Benjamin Gathiru Mejja Donk (Embakasi ya Kati), Kamau Munyoro (Kigumo), George Koimburi (Juja), Teresiah Wanjiru (Mteule), aliyekuwa mbunge wa kaunti ya Laikipia Cate Waruguru na aliyekuwa mbunge wa Mukurwe-ini Anthony Kiai, miongoni mwa wengine.