Home Habari Kuu Gachagua awaka moto, aapa makundi haramu yatakabiliwa vikali

Gachagua awaka moto, aapa makundi haramu yatakabiliwa vikali

0

Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa onyo kali kwa majaribio yoyote ya kufufua makundi ya uhalifu yaliyoharamishwa katika eneo la Mlima Kenya.

Amesema yuko tayari kugharimika kisiasa kuhakikisha makundi hayo yanakabiliwa kikamilifu.

Naibu Rais amesema serikali iko macho na itachukua hatua za haraka kusitisha majaribio ya viongozi wa makundi hayo na washirika wao kusajili vijana katika eneo hilo.

Amesema matendo ya kinyama yaliyotekelezwa na makundi hayo awali bado yamenata katika bongo za wakazi wa Mlima Kenya.

Ameonya kuwa hakuna yeyote atakayeruhusiwa kutumia vijana vibaya.

“Niko tayari kulipa gharama yoyote ya kisiasa kulinda wanawake hawa na wasichana wetu kutoka kwenye minyororo ya makundi ya uhalifu. Hatuwezi tukaruhusu hili,” aliapa Gachagua wakati akizungumza huko Nyandarua.

Aliongeza kuwa wale wanaojihusisha na majaribio hayo watakabiliwa kikamilifu kisheria.

 “Jaribio linafanywa kufufua kundi la uhalifu. Miezi miwili iliyopita, walirejea katika vituo vya mabasi wakiitisha pesa kutoka kwa wahudumu wa matatu na wafanyabiashara. Hatuwezi tukaruhusu yeyote kutumia vibaya vijana wetu na kujihusisha katika uhalifu. Tuna wajibu wa kulinda vijana wetu dhidi ya kutumiwa vibaya na mtu yeyote.”

Matamshi ya Gachagua yanakuja siku chache baada ya vijana zaidi ya 200 kukamatwa mjini Nyeri.

Vijana hao walikamatwa wakati wakijiandaa kuhudhuria mkutano uliotibuliwa na ulioitishwa na kiongozi wa zamani wa kundi la Mungiki Maina Njenga.

Baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya katika siku za hivi karibuni wamelalamika kuwa kunao wanaofanya juhudi za kufufua kundi la Mungiki.

Martin Mwanje & DPCS
+ posts