Home Habari Kuu Gachagua alalamikia ajali barabarani, ataka asasi husika kudumisha usalama

Gachagua alalamikia ajali barabarani, ataka asasi husika kudumisha usalama

0
Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa wito kwa watumiaji wa barabara, asasi za usalama na asasi husika kuhakikisha usalama unadumishwa barabarani ili kuepukana na ajali na vifo vinavyotokana na ajali hizo. 
Aliyasema hayo alipoitembelea familia ya Sammy Mwangi Gatumbo nyumbani kwao Chaka, Kieni, kaunti ya Nyeri, akiandamana na mkewe Dorcas Rigathi na viongozi wengine.
Familia hiyo ilipoteza jamaa sita kwenye ajali iliyotokea usiku wiki jana ikihusisha gari dogo na matatu kwenye barabara ya Nyeri-Nyahururu.
Jumla ya watu tisa walifariki wakati wa ajali hiyo wakiwemo watoto huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.
Naibu Rais aliitoa moyo familia hiyo kusalia imara, na pia kuwasilisha rambirambi za Rais William Ruto kwa familia hiyo.
“Naitembelea familia hii kama jirani na mwanachama wa jamii hii. Tutaendelea kuwaombea. Tunapaswa kusimama nanyi wakati huu mgumu kwa sababu kupoteza jamaa sita wa familia ni pigo kubwa,” alisema Gachagua.
Mkewe Dorcas aliwataka madereva kuwa waangalifu wanapokuwa barabarani.
Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, Seneta Wahome Wamatinga na mbunge wa Kieni Njoroge Wainaina ni miongoni mwa viongozi waliokuwapo.
Mamlaka ya Usalama Barabarani, NTSA inasema watu 3,609 walifariki kufuatia ajali za barabarani zilizotokea kati ya mwezi Januari – Octoba, 2023.
Website | + posts