Home Habari Kuu Gachagua akanya wanaoingilia siasa za Mlima Kenya

Gachagua akanya wanaoingilia siasa za Mlima Kenya

0

Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa onyo kali kwa wanasiasa fulani wa eneo la Bonde la Ufa ambao anasema wanaingilia siasa za Mlima Kenya.

Akizungumza jana huko Eldoret kaunti ya Uasin Gishu kwenye hafla ya kutawazwa kwa askofu wa kanisa katoliki John Kiplimo Arap Lelei, Gachagua alisema viongozi hao ambao wana ukaribu na Rais william Ruto wameanzisha siasa za urithi za mwaka 2032.

Kiongozi huyo aliongeza kusema kwamba viongozi hao tayari wanafanya mikutano na viongozi fulani wa ngome yake ya Mlima Kenya na kuzua migawanyiko katika eneo hilo.

Waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen ambaye alikuwa kwenye hafla hiyo alimjibu Naibu Rais akimhimiza kutotilia maanani kelele za siasa na badala yake kuangazia kazi yake.

kando na siasa Gachagua alipongeza kanisa kwa jukumu muhimu ambalo inatekeleza katika kutoa huduma za afya hasa mashinani akisema zinapiga jeki huduma zinazotolewa katika hospitali za umma.

Alisema zinasaidia pia kuhudumia watu hospitali za umma zinapokumbwa na changamoto kama mgomo wa hivi maajuzi wa madaktari.

Kuhusu malipo kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa waliowasilisha maziwa kwa kampuni ya New KCC, Gachagua alisema serikali tayari imetoa shilingi milioni 600 na hivi karibuni itatoa pesa za kununua mahindi kutoka kwa wakulima kupitia kwa bodi ya nafaka na mazao.

Naibu Rais kwa niaba ya Rais William Ruto na serikali nzima alimpongeza Askofu wa Dayosisi ya Eldoret John Kiplimo Lelei kwa kutawazwa.