Home Kimataifa Gachagua aitaka jamii ya Wamaasai kuepukana na tamaduni zilizopitwa na wakati

Gachagua aitaka jamii ya Wamaasai kuepukana na tamaduni zilizopitwa na wakati

0
Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa wito kwa jamii ya Wamaasai kupigia debe elimu ya watoto wasichana sambamba na ile ya wavulana na kuepukana na ndoa za utotoni.  
Akizungumza leo Jumatano katika eneo bunge la Narok Magharibi, Naibu Rais alisema tamaduni kama vile ndoa za utotoni na kukosa kuwapeleka watoto wasichana shuleni zimepitwa na wakati akiongeza kuwa serikali imedhamiria kuziangamiza ili kuhakikisha masomo kwa wote na kuwawezesha vijana.
“Wasichana ni sharti wapewe fursa ya kwenda shuleni na kuungwa mkono kutimiza ndoto zao,” alisema Gachagua wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kimkakati wa mwaka 2023-2027 wa eneo bunge hilo.
“Jamii ya Wamaasai lazima iachane na utamaduni wa ndoa za mapema kwani umepitwa na wakati. Hebu tuwekeze katika elimu ili wasichana waweze kuwa huru siku za usoni na kuwa wenye manufaa kwa jamii. Wasichana wanapaswa kuwa shuleni.”
Naibu Rais aliwaagiza maafisa wa utawala wa serikali kuu wakiongozwa na kamishna wa kaunti hiyo na machifu kuhakikisha tamaduni haramu na zilizopitwa na wakati zinatokomezwa, akiongeza kuwa ndoa za utotoni ni ukiukaji wa haki za watoto.
Miongoni mwa viongozi wanawake wa ngazi ya juu kutoka jamii ya Wamaasai ni Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabia Nchi na Misitu Soipan Tuya.
Naibu Rais alimsifia Tuya ambaye ni wakili kitaaluuma akimtaja kuwa kielelezo kwa wasichana katika jamii hiyo.
Website | + posts