Safari ya Harambee Stars kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka 2026, ilianza kwa nuksi ya kucharazwa magoli 2-1 na wenyeji Gabon katika uga wa Franceville Alhamisi jioni.
Masoud Juma aliiweka Kenya uongozini katika kipindi cha kwanza kabla wenyeji kusawazisha dakika ya 60 kupitia kwa Dennis Bouanga, na Guelor Kanga akafyatua fataki ya dakika ya 88 na kuwapa Panthers ushindi maridhawa.
Kenya watasafiri kwenda Ivory Coast kwa mchuano wa pili wa kundi F dhidi ya Ushelisheli Jumatatu ijayo, huku Gabon wakifunga safari ya Burundi.
Burundi wakicheza nyumbani pia waliilaza Gambia mabao 3-2 Alhamisi.
Ivory Coast itawaalika Ushelisheli katika mchuano wa kuhitimisha raundi ya kwanza kundi F Ijumaa jioni.