Chuma cha Naibu Rais Rigathi Gachagua yamkini kipo motoni kwenye Bunge la Taifa.
Hii ni baada ya wabunge wengi kusemekana kuazimia kuunga mkono hoja ya kumtimua Gachagua kwenye wadhifa huo.
Hoja hiyo inatarajiwa kuwasilishwa kwenye Bunge la Taifa linaloongozwa na Spika Moses Wetang’ula leo Jumanne alasiri.
Tayari, Wetang’ula ameashiria kuunga mkono hoja hiyo akisema kiongozi yeyote anayesababisha migawanyiko miongoni mwa Wakenya anapaswa kutimuliwa madarakani.
Ikiwa hilo litatimia, Gachagua atakuwa Naibu Rais wa kwanza kuwahi kutumuliwa na bunge kutoka kwenye wadhifa huo.
Aliyekuwa Makamu wa Rais wakati wa enzi ya Hayati Mzee Jomo Kenyatta, Jaramogi Oginga Odinga alijiuzulu kwa hiari baada ya kulalamika kuwa hakupewa majukumu ya kutekeleza na hivyo hakustahili kushikilia wadhifa huo na kulipwa fedha za umma kwa kazi ambayo hakufanya.
Ili kumtimua Gachagua kwenye wadhifa huo, wabunge wasiopungua 233 wanahitajika kuunga mkono hoja hiyo.
Kisha hoja hiyo itapelekwa kwenye Bunge la Seneti ambako angalau Maseneta 45 kati ya 67 wanapaswa kuiunga mkono.
Baadhi ya wabunge wanaoegemea upande wa serikali wamesikika wakidai wana idadi kubwa ya wabunge wanaounga mkono hoja hiyo kuliko idadi inayohitajika kikatiba.
“Naibu wa Rais anasema tunamuuzia uoga. Sisi hatuuzi wala kununua uoga. Tunafanya chenye tunajua ni right for this country. Kila nyani iko na siku yake na yako ndugu yangu Rigathi Gachagua, we are waiting for Tuesday,” alisema mbunge wa Mogotio Reuben Kiborek kuhusiana na njama ya kumfurusha Naibu Rais madarakani.
“Kwa minajili ya Kenya moja, tumeweka sahihi ya impeachment ya kumwondoa Naibu Rais. Hata wale watapitisha hiyo mswada siyo sisi, ni wenzake kutoka Mlima. The motion is already set and we are going to do what needs to be done and we hope the President will give us a person who is going to work with him,” aliongeza Florence Jematia, Mwakilishi wa Wanawake katika kaunti ya Baringo.
Gachagua amejipata matatani kutokana na kile wakosoaji wake wanasema ni kucheza siasa za kikabila wakati anapaswa kuwa akipigania kudumishwa kwa umoja wa taifa kwa mujibu wa wadhifa anaoshikilia.
Tofauti ambazo zimechipuka kati ya Rais William Ruto na Naibu wake zinawakumbusha Wakenya zile zilizoshamiri kati ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na William Ruto wakati huo akiwa Naibu Rais.
Ila kwa Ruto na Gachagua, ni tofauti ambazo zimechipuka miaka miwili tu baada ya wao kuwa madarakani, kinyume cha zile kati ya Uhuru na Ruto zilizoanza kutokota katika muhula wa pili wa utawala uliopita.