Taifa la China limeelezea dhamira yake thabiti ya kutoa msaada zaidi kwa nchi za Afrika katika vita vyao dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kabla ya Kongamano la 2024 la jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) mjini Beijing, maafisa wa juy wa serikali ya China wamesema kuwa nchi hiyo iko tayari kuunga mkono juhudi za bara hilo kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Akikiri kwamba China na Afrika zimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya hali ya hewa, Bw. Li Yonghong, ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa kituo cha ushirikiano wa mazingira cha nje katika wizara ya Ekolojia na Mazingira ya China, alisisitiza ahadi ya China ya kutoa msaada. Alieleza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa ni jambo la kimataifa ambalo linahitaji hatua za pamoja ili kushinda.
Bw. Li alitaja hatua kadhaa za China kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi barani Afrika kama ushahidi tosha wa ahadi yake. Alitoa mfano wa azimio la ushirikiano wa China na Afrika juu ya mabadiliko ya tabianchi, ambalo lilianzisha mchakato wa ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Afrika juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.
“Katika muktadha wa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, tumetoa misaada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mifumo ya satelaiti, vituo vya kupokea satelaiti ya hali ya hewa, vituo vya nguvu vya jua, taa za barabarani za jua, mifumo ya uzalishaji wa umeme wa jua, viyoyozi vya kuokoa nishati, na taa za kuokoa nishati za aina ya LED, zimeshatolewa,” alisema Bw. Li
Kwa mujibu wa Bw. Li, mipango hii imesaidia pakubwa kufanikisha juhudi za kujenga uwezo wa nchi za Afrika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Alidokeza kuwa China imetia saini mikataba ya makubaliano na takriban nchi 17 za Afrika kuhusu ushirikiano wa Kusini na Kusini juu ya mabadiliko ya hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na makubaliano juu ya ujenzi wa maeneo ya maonyesho ya kaboni ya kiwango cha chini katika baadhi ya mataifa barani humo.
Kando na hayo, alisema wataalam kutoka nchi za Afrika katika sekta ya mabadiliko ya hali ya hewa wameshiriki katika warsha mbali mbali nchini China ili kuongeza ujuzi wao juu ya mada hiyo.
Bw. Li pia aligusia pendekezo la China mwaka jana la mradi wa “ukanda wa mwanga wa Afrika”, ambao unalenga kukuza ushirikiano wa Kusini-Kusini juu ya mabadiliko ya hali ya hewa barani Afrika. Mradi huo unalenga kuunganisha rasilimali za bara la Afrika na kushughulikia mahitaji ya maendeleo ya nishati safi.
“Kupitia msaada wa vifaa, kubadilishana na mazungumzo, utafiti wa pamoja, na kujenga uwezo wa wataalam, China na Afrika zitaanzisha ukanda wa maonyesho kwa ushirikiano katika matumizi ya rasilimali za jua kusaidia nchi za Afrika kukabiliana na matatizo yao ya umeme,” alielezea Bw. Li.
Bw. Li alisema kuwa China itaendelea kuimarisha mawasiliano, uratibu, na ushirikiano wa vitendo na nchi za Afrika ili kuongeza uwezo wao wa kushughulikia masuala yanayohusiana na hali ya hewa. Aidha, alisema China itaendelea kutetea mfumo wa haki wa utawala wa hali ya hewa duniani.
Afisa huyo wa ngazi za juu serikalini alisema China itaipa kipaumbele masuala ya uzingatiaji wa malengo, kanuni, na mipango ya kitaasisi ya mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa na mkataba wa Paris. Bw. Li alisisitiza kuwa Beijing itahakikisha kuwa maslahi ya nchi zinazoendelea yanalindwa kupitia utekelezaji mwafaka wa Mkataba wa Paris.