Home Burudani Filamu ya matukio halisi kuhusu Bobi Wine kuzinduliwa

Filamu ya matukio halisi kuhusu Bobi Wine kuzinduliwa

0
kra

Filamu ya matukio halisi kuhusu kiongozi wa upande wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine imeandaliwa na itazinduliwa Julai 28, 2023 katika kumbi za maonyesho.

Filamu hiyo ambayo imepatiwa jina la “Bobi Wine: The People’s President” imeandaliwa na mtayarishaji filamu John Battsek kutoka Uingereza ambaye ameafikia ufanisi mkubwa katika nyanja ya filamu za matukio halisi almaarufu, “Documentaries”.

kra

Waelekezaji wa kazi hiyo ya sanaa ni wawili, Moses Bwayo mwenye makao mjini Los Angeles nchini Marekani na Christopher Sharp ambaye anaishi nchini Australia. Moses Bwayo alizaliwa nchini Uganda sawa na Christopher Sharp hata ingawa ni mzungu.

Watatu hao waliamua kuangazia jinsi Bobi Wine ambaye ni mwanaharakati, mwanamuziki na mwanasiasa, anahatarisha maisha yake nchini Uganda kupinga utawala wa Rais Yoweri Museveni.

Museveni ameongoza nchi hiyo tangu mwaka 1986 na alibadilisha katiba ya nchi hiyo ili kumwezesha kutafuta kuchaguliwa tena kwa kipindi cha miaka mitano.

Wine alitumia muziki kupinga utawala wa kiimla na kupiga jeki mpango wake wa kutetea wanyonge katika jamii nchini Uganda alipokuwa akiwania urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2021.

Alikabiliana pia na maafisa wa polisi na wanajeshi katika safari hiyo. Maafisa wa usalama walitumia mbinu mbaya kama vile mateso kujaribu kumnyamazisha Wine na wafuasi wake.

Mkewe Bobi Wine, Barbara “Barbie” Itungo Kyagulanyi ambaye ni mwandishi wa vitabu, mfadhili na mtetezi wa haki za binadamu ameangaziwa pia kwenye filamu hiyo pamoja na watoto wao.