Shirikisho la mawakili wanawake nchini FIDA, limejitokeza kulaani ongezeko la visa vya mauaji dhidi ya wanawake nchini pamoja na kulaumiwa kwa wanawake ambao wameuawa.
Wakihutubia wanahabari Jumanne jijini Nairobi, mawakili hao wakiongozwa na Mkurugenzi mkuu wa FIDA Anne Ireri na naibu mwenyekiti Christine Kungu, walisema wanasikitishwa sana na ongezeko la matukio ya ukatili dhidi ya wanawake hasa mauaji ya hivi majuzi ya Starlet Wahu Mwangi.
Wawili hao walisema kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kesi 10 za mauaji ya wanawake zimeripotiwa kwenye vyombo vya habari huku kesi nyingi zaidi zikiwa hazijaripotiwa.
Ireri pia amethibitisha kujitolea kwake kutoa uwakilishi wa kisheria bila malipo na usaidizi wa kisaikolojia kwa familia ya mwathiriwa.
FIDA pia imeomba serikali kuimarisha mifumo ya udhibiti wa vyumba vya malazi ambapo matukio ya hivi majuzi yameripotiwa.