Home Habari Kuu Fedha za El Nino? Sahau, Gachagua awaambia Magavana

Fedha za El Nino? Sahau, Gachagua awaambia Magavana

0

Naibu Rais Rigathi Gachagua amepuuzilia mbali madai ya Magavana kuwa serikali kuu haijawapatia fedha za kukabiliana na athari za mvua za El Nino zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini. 

Gachagua badala yake anawataka Magavana kutumia fedha za dharura katika bajeti zao na kutenga upya fedha katika bajeti hizo ili kuwahudumia watu ambao wanaowaongoza.

“Serikali kuu itatoa fedha kupitia timu za uratibu za kaunti, washirika wa maendeleo na mashirika ya kibinadamu pia yatatoa fedha kupitia kwa timu hizo, na tunazitarajia serikali za kaunti kufanya vivyo hivyo,” alisema Naibu Rais alipokutana na washirika wa kimaendeleo katika makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi leo Jumatano.

“Kwa hivyo, tunashangazwa kidogo tunaposikia magavana wakilalama kuwa hawajapata fedha za El Nino kutoka kwa serikali kuu. Fedha kama hizo hazitatolewa.”

Akiwahutubia wanahabari jana Jumanne, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir alikanusha madai kuwa serikali kuu imezipa kaunti shilingi bilioni 10 za kukabiliana na athari za mvua za El Nino akitaja madai hayo kuwa uongo mtupu.

“Kumekuwa na madai kuwa serikali kuu imezikabidhi kaunti shilingi bilioni 10 za kukabiliana na athari za mvua ya El Niño. Ili kuondoa mashaka, licha ya changamoto, serikali ya kaunti ya Mombasa imekabiliana na athari za mvua hiyo ikitumia rasilimali zake yenyewe na kwa kusaidiwa na Shirika la Msalaba Mwekundu, mashirika yasiyokuwa ya serikali na taasisi huru kwa mantiki ya nia njema,” alisema Gavana Abdulswamad wakati akiwahutubia wanahabari.

“Bunge na Mdhibiti wa Bajeti wanapaswa kuchunguza madai haya ya kutolewa kwa shilingi bilioni 10 na kuwabainisha raia ni wapi fedha hizi zilienda kwa sababu hazikupokelewa na kaunti.”

Gavana wa kaunti ya Siaya James Orengo aliyeandamana naye aliunga mkono msimamo huo.

Wakati malumbano hayo yakichacha, Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini inawataka Wakenya kujiandaa kwa mvua zaidi katika kipindi cha wiki moja ijayo.

Mvua za El Nino zinazoendelea kunyesha nchini zimesababisha mafuriko katika kaunti mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mombasa, Mandera na Wajir na kusababisha maelfu ya wakazi kuachwa bila makazi.

Kiasi kwamba wabunge wa bunge la taifa wanataka mafuriko kutangazwa kuwa janga la kitaifa.

 

Website | + posts