Shule za Highway, Musingu na vipusa wa Butere wameshinda mechi za pili hii leo Jumatano katika mashindano ya shule za upili ya Afrika Mashariki, FEASSSA yanayoendelea mjini Mbale nchini Uganda.
Kwenye mechi za usubuhi, Musingu na Highway walizilaza Kalangalala na Benjamin Mkapa za Tanzania kwa magoli manne na mawili kwa sufuri mtawalia. Magoli ya Musingu yalitiwa kimiani na Hamisi Otieno, Derrick Oketch aliyejifunga mawili na Elvis Kante.
Vile vile, kina dada wa St. Joseph ( Joga) nao walipata ushindi wa magoli mawili kwa yai dhidi ya Tanzanite (Tanzania) nao wavulana wa St. Joseph ( JOBO) wakatoshana nguvu ya sufuri kwa sufuri na wenyeji Bukedea (Uganda).
Wakati wa alasiri, mabingwa wa kitaifa – Butere walivuna ushindi wa kwanza wa magoli mawili kwa nunge dhidi ya Rines (Uganda). Mabao hayo yalitingwa na Joy Valencia na Patience Asiko.
Kwenye magongo, St.Antony ilishinda Kyadondo (Uganda) mabao matatu kwa moja nayo Musingu ikailaza Arusha Meru (Tanzania) magoli mawili kwa nunge.
Upande wa voliboli, Namwela iliipiku Bugobwa (Uganda) seti tatu kwa moja za 25:22, 25:19, 18:25 na 25:22 ,nayo Cheptil ikaizaba St. Augustine (Uganda) seti tatu. Vipusa wa Kwanzanze walio pia mabingwa watetezi, walishinda Seroma seti tatu kwa nunge za 25:18, 25:11, 25:16.
Katika raga ya wachezaji 15 kila upande, All Saints iliilaza Namilyango alama 13 kwa saba wakati Kitondo ikiizaba Kings College Budo (Uganda) alama 24 kwa 11. Butula iliipiku Maekere (Uganda) alama 31 kwa 25. Lenana ilishindwa na St. Mary’s College Kisubi (Uganda) alama 43 kwa yai.
Wakati huo huo, raga ya wachezaji 7 kila upande ilisakatwa. St. Joseph ilishinda Ninja SS – Uganda alama tano bila jibu nayo Nyagichenche ikalazwa alama 22 kwa tano na Noma (Uganda).
Kwenye uga wa vikapu vya wachezaji watatu kila upande, Butere iliizaba Mbinga ( TZ) vikapu 13 kwa 10 wakati Nasokol ikilemewa vikapu 14 kwa 11 na Ape Rugunga ya Rwanda. Pia Kimilili iliishindwa na Wampweo ( Uganda) alama 23 kwa 20 katika mchezo wa wavu.
Hapo kesho Alhamisi na kesho kutwa Ijumaa, soka itachukua mapumziko kupisha riadha ugani Amus, ila michezo mingine itaendelea kama kawaida.