Home Habari Kuu Faye aapishwa kuwa Rais wa Senegal, Rais Ruto ampongeza kufuatia ushindi

Faye aapishwa kuwa Rais wa Senegal, Rais Ruto ampongeza kufuatia ushindi

0

Rais William Ruto amempongeza Rais mpya wa Senegal Bassirou Diomaye Faye baada ya kuibuka mshindi wa uchaguzi mkuu ulioandaliwa nchini humo mwezi jana. 

Rais Ruto amesema wakati Rais Faye anaposhika hatamu za uongozi wa nchi hiyo, atafanya kazi pamoja naye kuimarisha ushirikiano kati ya Kenya na Senegal.

“Pongezi kwa Bassirou Diomaye Faye kufuatia ushindi wako mkubwa kwenye uchaguzi. Uongozi wako wenye maono unatia moyo na unaweka mfano usiokuwa na kigezo kwa viongozi wanaochipukia. Wakati unaposhika madaraka leo, tunaahidi kufanya kazi nawe kuimarisha uhusiano kati ya Kenya na Senegal kwa manufaa ya ustawi wetu sote,” alisema Rais Ruto katika ujumbe wake wa pongezi kupitia mtandao wa X.

Ruto alimpongeza Faye wakati ambapo ameapishwa kuwa Rais wa tano wa Senegal katika hafla iliyofanyika katika mji mkuu, Dakar.

Mapema mwezi huu, Faye mwenye umri wa miaka 44 alishinda uchaguzi uliocheleweshwa kwa kupata asilimia 54 ya kura zilizopigwa, mbele ya mpinzani wake mkuu Amadou Ba.

Ijumaa wiki iliyopita, Baraza la Kikatiba la nchi hiyo lilimthibitisha Faye kuwa mshindi.

Wakuu wa nchi kutoka bara zima walihudhuria sherehe za kuapishwa, akiwemo Bola Tinubu, Rais wa Nigeria na mwenyekiti wa kambi ya kikanda, Ecowas.

Martin Mwanje & BBC
+ posts