Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS imeapa kuwa maandamano yoyote yatakayofanywa kesho Jumatano yatakabiliwa vikali kwa mujibu wa sheria.
Inspekta Mkuu wa Polisi Japhet Koome anasema kinyume cha mahitaji ya sheria, hakuna yeyote aliyewataarifu polisi kuhusiana na kufanyika kwa maandamano hayo.
“Ingawa kifungu nambari 37 kinaruhusu kufanyika kwa maandamano, mafunzo yaliyotokana na maandamano sawia siku chache zilizopita yaliyosababisha uharibifu wa mali, majeraha na vifo yanaashiria bayana kuwa maandamano kama hayo ni tisho kwa usalama wa taifa,” Koome alisema katika taarifa leo Jumanne.
“Kwa mujibu wa mamlaka ya NPS ya kudumisha sheria na mpangilio, kulinda maisha na mali na kudumisha amani, tungependa kuutarifu umma kuwa maandamano yoyote yatakayofanywa katika sehemu yoyote ya Kenya kesho Jumatano, Julai 19 kuwa yatakabiliwa mara moja kwa mujibu wa sheria.”
Koome sasa anatoa wito kwa raia wanaotii sheria kuendelea mbele na shughuli zao za kila siku.
Inspekta Mkuu wa Polisi alitoa kauli hizo wakati muungano wa Azimio umeshikilia kuwa maandamano yake ya siku tatu yanayoratibiwa kuanza kesho Jumatano yataendelea kama ilivyopangwa.