Home Kaunti Familia yaomboleza Eldoret baada ya mwanao kufariki Canada

Familia yaomboleza Eldoret baada ya mwanao kufariki Canada

0
Marehemu Brian Kiprop
Marehemu Brian Kiprop

Familia moja mjini Eldoret inaomboleza kifo cha mwanao Brian Kiprop aliyekuwa akisomea shahada ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia katika Chuo Kikuu cha Winnipeg, Manitoba nchini Canada.

Mwili wa Kiprop ulipatikana ukielea mtoni nchini Canada.

Uchunguzi wa awali unaonyesha alikuwa na matatizo ya kisaikolojia kabla ya kifo chake.

“Nilipowasiliana naye wiki mbili zilizopita, nilihisi alitatizika kiakili kwani aliniambia anataka arejeshwe nyumbani mara moja,” alisema mama yake mzazi Hellen Limo.

Wakati wa mazungumzo kati yao, Limo anakumbuka mwanawe akimuomba dola 300 za Marekani ili akanunue simu ya mkononi baada ya simu yake kuloa maji.

Akizungumza na wanahabari nyumbani kwao huko Sogomo, Chepkoilel mjini Eldoret, mama yake huyo alisema familia bado haijaamini kuwa mwanao hayupo tena.

Marehemu Kiprop ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa shule ya upili ya Segero Adventist alikataa ofa ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Kisii baada ya kudahiliwa na Chuo Kikuu cha Kimataifa.

Familia ilitaarifiwa kupitia arafa kuwa mwili wa mwenda zake ulipatikana Julai 17 mwaka huu.

Familia sasa inasubiri ripoti ya kina kuhusiana na kifo cha mwanao kutolewa na polisi nchini Canada wakati ikichangisha karibu shilingi milioni 2.5 zinazohitajika ili kuurejesha mwili wa marehemu nyumbani.

Sasa inatoa wito kwa ubalozi wa Kenya nchini Canada na serikali ya Rais William Ruto kuingilia kati na kuisaidia kurejesha mwili wa mwanao nyumbani.

Taarifa ya Kimutai Murisha 

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here