Home Burudani Familia ya Lokassa ya Mbongo kumzika mwezi huu

Familia ya Lokassa ya Mbongo kumzika mwezi huu

0

Familia ya mpiga gitaa maarufu wa Congo Lokassa ya Mbongo huenda ikalazimika kuzika mwili wake bila usaidizi wa serikali ya nchi hiyo.

Hii ni baada yao kusubiri usaidizi wa serikali kwa muda mrefu na sasa ni miezi saba tangu kuaga dunia.

Mwili wa marehemu Lokassa umehifadhiwa kwenye makafani jijini Kinshasa baada ya kurejeshwa nchini humo kulingana na matakwa yake kwamba azikwe nyumbani kwao.

Mwanawe André Marie Lokassa aliambia BBC kwamba serikali ya Congo ilikuwa imeahidi kumwandalia hafla ya mazishi ya hadhi yake kutokana na mchango wake katika muziki lakini hadi sasa haijafanya hivyo.

Chama kimoja cha kusaidia wasanii kiliripoti kwamba mizozo katika familia ya marehemu ndiyo inakwamisha mazishi.

Afisa wa mawasiliano katika Wizara ya Utamaduni na Sanaa Magloire Paluku alikataa kuzungumzia suala hilo na badala yake kuelekeza wanahabari kwa familia.

Andre aliambia BBC kwamba familia iliwasilisha ombi la dola elfu 75 kwa serikali kugharimia mazishi ya babake, ombi ambalo halijajibiwa hadi sasa.

Alisema hali hiyo inasababisha mvutano kwenye familia.

Familia hiyo sasa inatumai kwamba itazika mpendwa wao mwezi huu wa Oktoba hata bila usaidizi wa serikali ikitizamiwa kwamba ada ya makafani pekee imezidi dola elfu 4.

Mpiga gitaa huyo maarufu ambaye jina lake halisi ni Denis Kasiya Lokassa, alifariki kutokana na maradhi ya kisukari na madhara ya kiharusi alichopata mwaka 2020.